Cignat Yapima Afya Bure Wanafunzi Dar

HOSPITALI ya Cignat Health System ya Sinza Kijiweni, imeanzisha zoezi la kupima afya bure wanafunzi wa shule za msingi ikiwa ni mchango wake kwa jamii. Zoezi hilo ambalo kwa kuanzia limepima wanafunzi zaidi ya 200 wa darasa la kwanza katika shule za msingi Mugabe na Mapambano na viziwi 14.

Zoezi hilo lina lengo la kuwakumbusha wazazi wajibu wao kupima afya za watoto wao na wanafunzi kudai haki ya kupimwa afya mara kwa mara, ili waweze kuhudhuria masomo bila kukosa.

Akizungumzia zoezi hilo, Mkurugenzi wa Cignat, Jannet Kumwembe, alisema: "Lengo ni kuikumbusha jamii umuhimu wa kupima afya mara kwa mara. Hasa kwa wanafunzi ili wasishindwe kwenda shule kwa matatizo ya afya."

Alisema ni muhimu kwa walimu pia kuwafuatilia wanafunzi wanashindwa kufika shule mara kwa mara kwani huenda wakawa na matatizo ya kiafya wakashindwa kuyasema bila kudadisiwa.

Katika Shule ya Msingi Mugabe watoto 97 wa darasa la kwanza na wengine 15 wenye mahitaji maalumu walipimwa afya ya kinywa, macho, masikio na ngozi.

Naye, Rais wa Cignat Health System, Dk Alex Kumwembe alisema kuwa, taasisi yake imeamua kupima afya bure kwa wanafunzi wa shule za msingi ikiwa ni mchango wake kwa jamii.